19 Machi 2011 - 20:30

Mkuu wa Taasisi ya Anga za Juu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatua za awali za kutuma satalaiti nyingine katika anga za mbali zimeshaandaliwa; na Tehran inataraji kuwa itatuma satalaiti nyingine katika kipindi cha miezi michache ijayo.

Ripoti ya ABNA- Bw. Fazeli amesema hayo katika sherehe za kuwapongeza wasomi na watafiti wa Kiirani katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Khoje Nasruddin Tusi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, satalaiti hiyo inatarajiwa kutumwa katika kilele cha sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu zinazofanyika februari 11 kila mwaka.
Amesema, ana matumaini zoezi la kurusha satalaiti hiyo litafanyika kwa mafanikio kama ilivyojiri kwa satalaiti za huko nyuma za Iran.
Mwezi Juni mwaka jana, Iran ilituma satalaiti inayojulikana kwa jina la Rasad katika anga za mbali ikiwa imetengenezwa na wanasayansi wa hapa Iran bila kutegemea msaada wa kigeni.
Rasad ni satalaiti ya kwanza ya Iran yenye uwezo wa kupiga picha kutoka anga za mbali.
Itakukmbukwa pia kuwa mwaka 2009 Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza ijulikanayo kwa jina la Omid yaani, Tumaini.